Sunday, November 28, 2010

Maria apatiwa Wheelchair

SIKU chache baada ya makala inayoelezea maisha ya Maria patrick na kuchapishwa kwenye gazeti la Tanzania Daima. Wasamaria wema wamejitokeza kumsaidia mtaji endapo atafungua account,
Tunaendelea kupokea ushauri na misaada kwaajili ya kumwezesha maria namba yake ni simu ni . 0654739656

Maria Patrick: Ninatambaa kwa shinda, ninaomba msaada wa baiskeli

*Ni fundi shereheni anayeshona kwa kutumia mikono
*Anahitaji, Baiskeli na mtaji wa kushona
Na Deogratius Temba
“NILIANZA kazi za ufundi wa kushona  mwaka 2004, pele mbagala misheni, kutokana na mimi kuwa mlemavu wa miguu, nikashindwa kutambaa hadi kule nikaamua kuacha  nitafute kitu kingine cha kufanya”
Huyo ni Maria Patrick (pichani)mkazi wa mtaa wa Nzansa A, Mbagala Charambe ambaye ni mlemavu wa miguu anayetembea kwa kutambaa chini kutokana na kupooza tangu akiwa mtoto mdogo.
Maria ni mama wa mtoto mmoja, Said Suleiman(12) ni fundi Cherehani,  anaujuzi wa kushona nguo mbalimbali kwa kutumia mashine ya cherehani yakusukuma kwa  mikono,  lakini kutokana na changamoto zinazotokana na ulemavu huo, anashindwa  kujishughulisha ipasavyo katika kutafuta wateja ili apate kipato cha kumwezesha kuishi na mtoto wake asome.
Maria anaeleza kuwa mwaka 2007 alikutana na Mwenyekiti wa Kikundi cha Mtandao wa walemavu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, (NEDPHA+),Spenciosa Mwakina. Kikundi hiki cha Mbagala ndani yake kuna walemavu wasio na VVU, ambao wamejiunga kwa lengo ni kupunguza umasikini kwa watu wenye ulemavu na kuwafanya wasiwe ombaomba.
Anaeleza kuwa baada kujiunga na NEDPHA+ kikundi kinachojengewa uwezo na semina za maendeleo ya Jinsia(GDSS) zinazoendeshwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP), amejiendeleza zaidi kiujuzi wakati anapokutana na wenzake kwenye kikundi, na zaidi  kuwafundisha walemavu wenzake ambao ndio wanaanza kujifunza ufundi wa kushona.
“kinachonisaidia zaidi mimi ninamashine yangu mwenyewe nyumbani, inanisaidia sana katika kufanya mazoezi na pia kujipatia kipato kidogo cha kuitunza familia yangu. Nilinunuliwa mashine hii na kaka yangu lakini sikuwa naelewa vitu vingi, nilipojiunga na NEDPHA+ nimejifunza mambo mengi na sasa mimi ni fundi kamili ninaweza kushona nguo za aina mbalimbali.
“Changamoto ninayokumbana nayo hivi sasa ni kushindwa kushirikia na wenzangu kutokana na kuwa siwezi kutembea, ninavyotambaa ninapata shida sana hadi kufika barabarani ili nipande daladala”anaeleza Maria na kuongeza:
“Wakati mwingine ukisema utapanda daladala nani atakubeba akupandishe na kukushusha? huna uhakika, sasa nikifikiria hilo inabidi nisiende kabisa nibaki nyumbani,”anaeleza Maria.
Anasema kuwa kutokana na yeye kutokuwa na uwezo wa kutembea, anahitaji baiskeli ya matairi matatu, itakayomsaidia kwenda sokoni kuuza nguo anazoshona, kuhududhuria mafunzo zaidi kwenye kikundi  chake na hata kushiriki semina mbalimbali ambazo zinaweza kumjengea uwezo zaidi.
“Natamani semina nyingi, lakini siwezi kushiriki kutokana na kutambaa, mvua ikinyesha huwezi kutoka ndani , hata wakati wa vumbi, inanisumbua kwasababu ninapatwa na kikohozi cha vumbi  ninapotambaa chini,”anaeleza na kuongeza:
“Mimi sikupenda kuwa ombaomba, kutokana na ulemavu nilionao ningeweza kukaa mahali nikaomba lakini bado ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa amenipa akili, mikono na nina afya nzuri, kukosa miguu tu hakunifanyi mimi nijione kuwa ndiyo mwisho wa kuwajibika, tatizo langu kubwa ni kupata usafiri wa kuitoa hapa nyumbani nikazunguke kutafuta wateja wanguo’ anaeleza Maria.
Maria anaomba wasamaria wema wamsaidie apate usafiri yaani Baiskeli ya matairi matatu ili aweze kujishughulisha na biashara ndogondogo, Mbali na hilo Maria anaomba  msaada wa mtaji kwaajili ya kupanua biashara yake ya kushona nguo kama kunua vitambaa vya kushona, vitenge na nyuzi.
Anasema: “ Ninashida hiyo ya mtaji, ili nipate kitu cha kumsaidia mtoto wangu huyu asome, anahitimu shule ya msingi mwaka 2010, atakwenda sekondari ni lazima nijitahidi kukusanya chochote ili aende shule,”
Kuhusu usafiri aliokuwa akiutumia awali, Maria anasema:“Nilikuwa na baiskeli yangu binafsi niliyokuwa nimepewa lakini kwasasa imekufa kabisa haitengenezeki tena, sasa hizi huwa ninaazima ya dada mmoja mbaye mara nyingi huwa hatiki kwahiyo ananipatia mimi ninapotaka kutoka, lakini hii inanikwamisha kwasababu sipo huru kutoka au kwenda mbali kwasbaabu anaweza kuhitaji baiskeli yake na akaikosa,”
Maria anaomba msaada kwa mtu yoyote mwenye chochote, amsaidie ili aweze kujikwamua na umasikini na aweze kujitegemea.
Kwa yoyote mwenye chochote, ushauri au nia ya kumwezesha Maria anaweza kutumia namba hizi 0715686575 au kufika katika ofisi za Mtadao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Mabibo Dar es salaam, kwa maelezo zaidi.