Pembezoni Mwa Pembezoni
Monday, October 24, 2011
Kilimo kwanza kinawanyonya wanyonge
*Wanaonufaika nacho ni makampuni makubwa
*Kinaongeza utegemezi na umasikini kwa wakulima masikini
Na Deogratius Temba
Katika kuhakikisha Tanzania inakuwa Taifa lenye kufuata haki ,usawa wa kijinsia katika umiliki wa rasilimali zake, ni lazima kuhakikisha jamii inanufaika na mipango na sera za serikali katika kupata maisha bora na endelevu.
Upo muhimu mkubwa wa jamii kufanya uchambuzi wa kina kupitia na kutoa maoni yenye mtazamo wa Kijinsia na haki kwa kila raia katika sera ya KILIMO KWANZA, na Ajira, maisha endelevu na biashara.
Katika uchambuzi wananchi wanapaswa kuelewa faida na hasara zizliopo katika kila mpango au sera. Mpango ya Kilimo iendane na uhalisia wa wananchi wa taifa hili, masikini na tajiri wote wapate sawa. Tunajua kuwa kwa miaka mingi iliyopita serikali imekipuuza KILIMO, nah ii imesababisha kupotea kwa ajira na watanzania kugeuzwa kuwa watumwa, manamba na kunyanyaswa na wawekezaji.
Hili ni suala la mapambano kuhusu utu na uhai wetu, adhari za kupoteza ajira ni kugeuzwa kuwa watumwa, na kudharauliwa na wawekezaji. Tujiulize nani atatuondoa katoka kwenye minyororo hii?
Mataifa ya Ulaya na Amerika yamefilisika kutokana na mitikisiko ya kifedha, yamehamia Afrika kuongeza uporaji ili kukuza mitaji yao iliyopotea. Tuimarishe mijadala ya kijamii vijijini bila kuogopa ili kila mtu adai haki yake.
Jamii kujitahidi kupata taarifa sahihi na kwa wakati kwa kushiriki katika mijadala ya pamoja vijijini au katika mitaa yao, ili kujua ni kitu gani kinaendelea katika taifa hili na kuweza kupaaza sauti zao na kudai haki, hasa wakishiriki katika kutumia fursa za kutoa maoni yao. Kutokuwa na taarifa za kutosha kunaweza kukusababisha kukosa fursa zilizopo katika nchi yako na ukashindwa kukubali au kukosoa.
Mchambuzi na mwanaharakati wa Chuo Kikuu cha Mzumbe,Profesa Aida Isinika, akichambua sera ya kilimo anasema: “ uwekezaji wa serikali kwenye kilimo ni mdogo sana ni wa maneno kuliko matendo kwani kasi ya kiutendaji katika kupunguza umasikini ni ndogo. Ni lazima kuongeza utendaji na kuweka mikakati endelevu inayotekelezeka”
Katika sekta binafsi fursa zipo kwenye mikopo, wakati dirisha dogo linalotajwa kuwa lipo katika benki ya rasilimali Tanzania(TIB) mkulima mdogo hawezi kwenda kukopa hapo kwani kiasi cha kukopa ni kuanzia Sh. Milioni 100 hadi Bilioni 1, na uweke amana ambazo mkulima mdogo hawezi kumiliki kama hati za nyumba, mashamba makubwa na vitu vingine.
Katika mchakato huu, KILIMO kwanza kimeonekana kama ni ajenda ya watu wakubwa wenye mitaji kwasababu, nguzo ya kwanza ya sera hiyo ni kuleta mapinduzi katika kilimo na kusababisha mapinduzi ya kijani. Wakati miundombinu ya barabra ni mibovu, kutoka shambani ili kufikia masoko ni tatizo kubwa.
Katika uchambuzi huo, Profesa Isinika anaainisha kuwa, kuna umuhimu mkubwa wa kilimo nchini Tanzania hasa kile cha wazalishaji wadogo. Asilimia 74 ya ajira zote zinatokana na kilimo, asilimia 95 ya chakula kinachotumia hapa nchini kinatokana na wakulima wadogo, asilimia 30 ya biadhaa zinazouzwa nchi za nje zinataka kwao, asilimia 65 ya malighafi zinazotumika viwandani hapa nchini.
Asilimia 9o ya chakula kinachozalishwa kinatokana na wakulima wadogo wakati asilimia 99 ya ardhi inayolimwa hapa nchini inalimwa na wakulima wadogo wanawake wakiwa ni nusu ya wakulima wadogo.
Pia katika kuzalisha, KILIMO KWANZA kinataka kuwepo na viwanda vya mazao, wakati Taifa linatatizo kubwa la upatikanaji wa umeme wa uhakika, mikoa mingi ya wilaya zinazolima kama vile Namtumbo, Mbinga na Songea Vijijini hawana nishati ya umeme ya Gridi ya Taifa, kwani wakati mafuta ya mitambo yakipanda bei kila mara wao bado wanatumia umeme wa majenereta yanayotumia mafuta.
Mwanaharakati wa ngazi ya jamii, Amina Mcheka, anasema kuwa sera ya kilimo kwanza haijamsaidia mkulima wa chini, maeneo ya kulima yenye mapori yameachwa bila kuwagawia wananchi, wakulima ambao wanamiliki ardhi nzuri wananyang’anywa na kupewa wawekezaji.
Profesa Marjone Mbilinyi, anasema kuwa serikali inatakiwa kuweka ajira kuwa kipaumbele kwani hatuwezi kuzungumza habari ya kupunguza umasikini bila kuzungumzia ajira. “Katika kilimo wafanyabiashara wakubwa wamekuja na mbegu zilizopunguzwa vinasaba, wafanyabiasahara wa makampuni makubwa wamegeuka kuwa wauaza mbolea, pembejeo za kilimo, dawa; hii inaonesha jinsi ambavyo mfumo wa ubepari umeingia kwenye kilimo na kusababisha tabaka kubwa”
Mkulima kutoka katika Muungano wa Vikundi vya wakulima(MVIWATA) mkoani Morogoro Tom Laizer, anasema kuwa mpango wa kilimo kwanza umezinduliwa bila kuwaeleza wananchi jinsi ya kupata taarifa na fursa za kilimo. Wanaopata ni wawekezaji pekee. Neno “Mapinduzi ya kijani” ni neno ngumu ambalo sii kila mkulima wa kijijini anaweza kulizungumzia. “ Kilimo kwanza ni mpango wa kuwafukuza wakulima wadogo masikini kutoka kwenye ardhi yao na kuwapatia wageni, kwani kwa miaka ya hivi karibuni inaonekana kuwa migogoro ya ardhi inaongezeka” anasema Laizer.
Makampuni makubwa yanayowekeza kwenye kilimo ndio wamekuwa wananunuzi wa kubwa wa mazao yanayozalishwa kwa kulangua, mabenki makubwa pia yameonesha kunufaika zaidi kuliko mwananchi masikini kutokana na kudai riba kubwa katika mikopo ya kilimo hasa hiki cha uzalishaji wa mbegu.
Mfumo huu wa mbegu za ‘Genetic Modified’ (GM) umekuwa kikwazo kwa wakulima wadogo kwa sababu hawawezi kuhifadhi mazao yao ili kuandaa mbegu kwa ajili ya msimu unaofuata, kwa hiyo unawalazimisha wakulima wadogo kuendelea na mtindo wa kununua mbegu madukani kila mwaka badala ya kuzalisha za kwao kwa njia za asili.
Madhara mengine ni matumizi ya zana kubwa katika kilimo kinachotumia mitambo na mafuta, hivyo kusababisha makampuni makubwa ya mafuta kujiingiza humo, kama wanufaika wakubwa na hivyo kujenga nguvu kubwa ya ushawishi ya kuendeleza aina hii ya kilimo.
Kilimo kwanza kinahitaji kuangaliwa upya ili uwe ni mpango wa wakilima wote masikini na matajiri, bila kubagua makundi yaliyoko pembezoni. Mpango wa KILIMO KWANZA ulenge kubadili hali ya maisha ya watu sio kuwaongezea mzigo wa maisha kwa nujiingiza kwenye gharama kubwa za ununuzi wa pmbejeo kubwa na dawa za kilimo.Tunahitaji mabadiliko! Deojkt@yahoo.com/0715686575
Monday, January 31, 2011
Subscribe to:
Posts (Atom)